Halmashauri ya Jiji la Mbeya iko mbioni kununua mashine tano za kisasa za kunawia mikono, ahadi hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Kamishna msaidizi wa Polisi James Kasusura wakati akipokea mashine moja ya kisasa ya kunawia mikono iliyonunuliwa na Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili kusaidia Wilaya ya Mbeya katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa covid -19.
Tukio hilo la kukabidhiwa mashine hiyo limefanyika asubuhi ya tarehe 08/04/2020 katika stendi kuu ya Mabasi Mbeya, huku wawakilishi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, kupitia kiongozi wao wa msafara ndugu Anyatike Mwakitalima wakiishukuru Halmashauri ya Jiji la Mbeya na Wilaya ya Mbeya kwa namna inavyopambana katika kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.
“Ndugu zangu tumekuja kuwaunga mkono katika mapambano dhidi ya corona kwani tumeona jitihada kubwa mnazozifanya kwa kushirikiana na uongozi wa wilaya yenu ndo maana tumenunua mashine hii ili iweze kusaidia katika mapambano haya ya corona” alisema Mwakitalima.
Wakati anapokea Mashine hiyo Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Kamishna msaidizi wa Polisi James Kasusura amefurahishwa namna mashine hiyo inavyofanya kazi bila ya kugusa mahali popote wakati wa unawaji wa mikono na sabuni, kitu ambacho kilimfanya atoe ahadi ya kuagiza mashine nyingine tano zitakazosaidia wananchi wa Jiji la Mbeya katika mapambano dhidi ya corona.
“Mashine hii ni nzuri na imetengenezwa hapahapa Mbeya na wenzetu wa Chuo kikuu cha Sayansi na tecknolojia Mbeya (MUST) ili kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa wa corona katika Jiji letu na nchi yetu kwa ujumla” alisema Kasusura.
Wakati huohuo mkurugenzi wa Jiji la Mbeya amewatakia kheri ya sikuu ya Pasaka wananchi wote wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya na kuwaambia kuwa Pasaka bila corona inawezekana.
Akizungumzia msaada huo Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe: William Paul Ntinika ameishukuru Wizara kwa jitihada kubwa inayoifanya katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa covid 19 ambao umekuwa ukienea kwa kasi kubwa Duniani kote.
Aidha Balozi wa kampeni ya nyumba ni choo ndugu Mrisho Mpoto amewataka wananchi wa Jiji la Mbeya kutokuchoka katika zoezi la kunawa mikono kwani ndio njia pekee na kubwa ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa covid 19
Mara baada ya kupokea mashine hiyo Mkurugenzi Kasusura alikabidhi mashine hiyo kwa mwenyekiti wa Stendi kuu ndugu Salumu ili iweze kutumiwa na watu wote wanaoingia stendi kuu ya mabasi Mbeya na kumtaka mwenyekiti huyo kutumia mashine hiyo kwa matumizi ya stendi ili kuwakinga wananchi wote wanaotumia stendi hiyo.
Nae mwenyekiti wa Stendi kuu ya Mbasi Mbeya ndugu Salumu ameishukuru serikali kwa kuwajali wananchi wa stendi kuu ya mabasi ya Mbeya kwa kuwapa mashine ya kisasa ya kunawia mikono” niwashukuru sana serikali kwa niaba ya maafisa usafirishaji wote wa stendi kuu kwa namna mlivyotujali na kutufanya tuwe wa wa kwanza kupokea mashine hii” alisema mwenyekiti Salum
Diwani wa Kata ya Sisimba ndugu Geofrey Kajigiri akiishukuru serikali kwa msaada huo kwa wananchi wake huku akiwaelezea wananchi furaha yake kwani bila afya kazi zao za stendi hazitaweza kwenda vizuri.
Serikali imekuwa katika mipango madhubuti ya kuhakikisha wananchi wake wanakuwa salama katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa corona ambao umekuwa ni tishio katika Dunia.
Mbalizi Road near TTCL Offices
Anuani ya Posta: 149 Mbeya
Simu: +25525252502372
Simu ya Kiganjani: +255 25 2502563
Barua Pepe: cd@mbeyacc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya City Council . All rights reserved.