Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya wameridhia kwa pamoja mchakato wa uanzishwaji wa Halmashauri mpya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya, ridhaa hiyo imetolewa katika Mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya ulioketi siku ya tarehe 29/01/2021 katika ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Mbeya wa Mkapa.
Akiwasilisha taarifa ya Kamati Maalumu ya uanzishwaji wa Halmashauri mpya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya iliyoundwa na Kamati ya fedha na Utawala ya Halmashauri hiyo, Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya ndugu Amede E.A, Ng’wanidako aliwaeleza wajumbe wa Mkutano wa Baraza kuwa taratibu za uanzishwaji wa Halmashuri mpya ndani ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa zipo kwa mujibu wa ibara ya 145 (1) na 146 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1997 na sheria namba 8 ya serikali za mitaa za mwaka 1984 sura 288.
Mkurugenzi Amede aliendelea kueleza kuwa hatua za uanzishwaji wa Mamlaka za serikali za Mitaa zimeanishwa katika mwongozo wa uanzishwaji serikali za Mitaa za mwaka 2014 uliotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Mwongozo huo umefafanua zaidi utaratibu wa kuanzisha Mamlaka ya Mji au kupandisha hadhi maeneo ya Utawala.
Aidha ndugu Amede alisema kwamba wajumbe walioteuliwa katika Kamati hiyo ni pamoja na Mheshimiwa Daudi Ngogo- Mwenyekiti, Mheshimiwa Dormohamed Issa Rahmat – Mjumbe, Mheshimiwa Agness Mangasila – Mjumbe, Mheshimiwa Daktari Tulia Ackson – Mjumbe, Mheshimiwa Ibrahim Mwampani- Mjumbe, Mheshimiwa Daniel Mwaibindi – Mjumbe, Mheshimiwa Adam Simbaya – Mjumbe pamoja na wataalamu ambao ni
Ndugu Amede E.A, Ng’wanidako, Mashaka Semkiwa, Dickley Nyato, Triphonia Kisiga, Oscar Kapinga , Adon Hajayand na Gerald Ruzika.
Majina ya waliopendekezwa katika kamati hiyo ni majina ya Madiwani kutoka Kamati ya Fedha na utawala ambao ni Mstahiki Meya , Naibu Meya na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini kwa nafasi zao, wengine ni wenyeviti wa Kamati za Mipangomiji na Ardhi na Kamati ya Uchumi ,Afya na Elimu na wajumbe wawili wa kuteuliwa ambao wanatoka kila kamati kwa kuzingatia uwakilishi wa Tarafa mbili za Iyunga na Sisimba.
Mchakato huu wa uanzishwaji wa Halmashauri mpya ndani ya Jiji la Mbeya unatokana na ahadi iliyotolewa katika ziara za kampeni na Mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha Mapinduzi ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Daktari John Pombe Magufuli mnamo tarehe 30, Septemba, 2020 na kusisitiza kuwa iwapo atachaguliwa kuwa Rais ataligawa Jiji la Mbeya na kuwa na Halmashauri mbili na kuagiza kikao cha kwanza cha Baraza pamoja na mambo mengine kijadiri mchakato wa uanzishwaji wa Halmashauri mpya.
Mbalizi Road near TTCL Offices
Anuani ya Posta: 149 Mbeya
Simu: +25525252502372
Simu ya Kiganjani: +255 25 2502563
Barua Pepe: cd@mbeyacc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya City Council . All rights reserved.