HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya, inatarajia kutumia zaidi ya Sh. Bilioni 88.3 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na matumizi mengine ya jiji hilo katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 huku makusanyo ya ndani yakitarajiwa kuongezeka.
Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Amede Ng’wanidako amesema hayo kwenye Mkutano Maalumu wa Baraza la Madiwani la kupitia na kujadili makadirio ya mapato na matumizi ya Bajeti ya Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Ng’wanidako amefafanua kuwa katika bajeti hiyo makusanyo ya ndani ya Halmashauri yataongezeka kutoka Sh. Bilioni 16.7 mpaka Sh. Bilioni 18.3 na kwamba makusanyo hayo yanatarajiwa kuongezeka kutokana na ongezeko la vyanzo vya mapato ambapo kwenye bajeti hiyo vimewekwa vipaumbele nane ambavyo fedha hizo zitaelekezwa kwenye ujenzi wa shule mpya na ukarabati wa zile zilizochakaa.
Aidha Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya ameweka bayana kuwa katika bajeti hiyo Halmashauri inakusudia kununua gari moja maalumu kwa ajili ya kuzolea taka, kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa mujibu wa sheria za nchi.
Pia amesema kuna mipango ya kujenga kituo kimoja cha afya ambacho kitajengwa katika Kata ya Isyesye na ujenzi wa shule moja maalumu ya Sekondari kwa ajili ya wanafunzi wa kuanzia Kidato cha kwanza mpaka kidato cha nne.
“Vipaumbele hivi na bajeti yetu nzima ni kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma bora kwa jamii yetu, ili tufanikishe haya ni lazima tuwe na ushirikiano wa kutosha baina ya madiwani na watumishi wote wa Halmashauri yetu, amesema Ng’wanidako.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Mheshimiwa Dormohamed Issa ameeleza mchakato wa Uandaaji wa Bajeti ulianza kabla ya kikao hicho ambacho kilikuwa cha mwisho kwa ngazi ya Baraza la Madiwani lilitanguliwa na vikao mbalimbali ambavyo ni Kamati za madiwani na watumishi na kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya ambayo pia iliridhia bajeti hiyo ipitishwe.
Mbalizi Road near TTCL Offices
Anuani ya Posta: 149 Mbeya
Simu: +25525252502372
Simu ya Kiganjani: +255 25 2502563
Barua Pepe: cd@mbeyacc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya City Council . All rights reserved.