Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Innocent Bashungwa amewataka wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanamaliza miradi yote ya ujenzi wa vituo vya afya na hospitali ifikapo April 30 mwaka huu kinyume na hapo hatua za uwajibishwaji zitafikiwa dhidi yao.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Hospitali ya Jiji la Mbeya Mhe: Bashungwa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amekuwa akibuni mbinu za kupata fedha ili kuboresha sekta ya afya hivyo wasaidizi wake hatutakiwi kumuangusha katika usimamizi na utendaji.
Aidha Waziri huyo amefafanua kuwa Halmashauri ambayo haitakamilisha ujenzi huo kwa wakati, hawatapewa fedha za kuendeleza ujenzi na Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi Watendaji watachukuliwa hatua za kinidhamu na amewataka Wakuu wa Mikoa kusimamia maelekezo hayo.
Pamoja na hayo Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa amewaelekeza wakurugenzi watendaji kuhakikisha Majengo yote ya kutolea huduma, yaliyokamilika katika maeneo mbalimbali nchini, yaanze kutoa huduma kwa wananchi, na sio kuyaacha kama magofu watakaobainika kuwa majengo yameisha na hawatoi huduma watachukuliwa hatua.
Hadi kufikia tarehe 15 Februari, 2022, vituo 110 kati ya 233, vilivyopokea fedha, vilikuwa vimekamilika na vimekwishapelekewa fedha ya awamu ya pili, jumla ya shilingi bilioni 27.5, kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa majengo ya wodi ya wazazi,upasuaji,kufulia na njia za waenda kwa miguu.
Waziri Bashungwa ameongeza kuwa Utaratibu huo ndio utakaotumika kwenye Miradi yote ya Afya msingi, na Halmashauri husika kama haijakamilisha ujenzi wa majengo ya awali yanayotakiwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi Watendaji watatakiwa kujibu kwa nini wasichukuliwe hatua za kinidhamu.
Mbalizi Road near TTCL Offices
Anuani ya Posta: 149 Mbeya
Simu: +25525252502372
Simu ya Kiganjani: +255 25 2502563
Barua Pepe: cd@mbeyacc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya City Council . All rights reserved.