Halmashauri ya Jiji la Mbeya imetoa kiasi cha Shilingi Milioni 200 ya Mapato yake ya ndani ujenzi wa kituo cha Afya Kata ya Ilemi Mtaa wa Masewe ambacho kwa awamu ya kwanza na ya pili kinatarajiwa kugharimu kiasi cha Shilingi 524,660,215.50.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Ndugu Amede E.A, Ng’wanidako amesema kiasi hicho cha fedha tayari kimeshawekwa kwenye akaunti ya Kata ya Ilemi tayari kwa ujenzi wa kituo hicho, na kubainisha kuwa fedha hizo ni sehemu ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya na kuwahakikishia wananchi wa Kata hiyo kuwapekekea fedha zaidi ili kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.
Nae Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya katika hotuba yake alieleza mipango ya serikali ni kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wake na ndio maana Halmashauri ya Jiji la Mbeya imetoa kiasi hicho cha fedha na itaendelea kutoa ili huduma ziwe karibu na wananchi.
Kaimu katibu tawala wa Wilaya ya Mbeya ndugu Vincent Mbua kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mbeya amewasihi wananchi hao kushirikiana katika ujenzi huo ili kukamilisha kwa wakati na kuwaomba wananchi hao kuwa walinzi wa mradi huo ili usiingie doa kwa matukio yasiyo na tija kama wizi na upotevu wa mali za mradi huo.
Akizindua ujenzi wa kituo hicho Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewasihi wananchi wa Kata hiyo kujitolea katika ujenzi wa kituo hicho cha Afya kwani ni mali yao “Ndugu zangu kituo hiki ni mali yetu sote hivyo kila mwananchi anawajibu wa kuchangia ujenzi wa kituo hiki kwani kitasaidia kutoa huduma ndani ya Kata yetu pamoja na Kata jirani “ alisema Dkt Tulia.
Aidha Dkt Tulia aliongoza Harambee na kufanikisha kupatikana kwa mifuko 274 ya Saruji huku Ofisi yake ikichangia mifuko 100 ya saruji na kutanabaisha kuwa mifuko hiyo ya saruji itapelekwa eneo la ujenzi ili kusaidia ujenzi wa kituo hicho, huku akiwataka waliotoa ahadi katika harambee hiyo kukamilisha ahadi zao ndani ya miezi mitatu
Katika ujenzi huo wa kituo cha afya wananchi wao wamejitolea nguvu kazi kwenye kuchimba msingi na shughuli nyingine zinazohusu ujenzi huo ikiwemo ung’oaji wa visiki pamoja na kusawazisha eneo la mradi
Ujenzi wa kituo hicho unataraijiwa kukamilika ndani ya miezi sita ili huduma zianze kutolewa kwa wananchi.
Mbalizi Road near TTCL Offices
Anuani ya Posta: 149 Mbeya
Simu: +25525252502372
Simu ya Kiganjani: +255 25 2502563
Barua Pepe: cd@mbeyacc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya City Council . All rights reserved.