Halmashauri ya Jiji la Mbeya imeuza mali zake chakavu kupitia mnada wa hadhara ulioendeshwa na mhakiki mkuu wa mali za serikali kwenye karakana ya Jiji ,Shule ya sekondari Mbeya na shule ya sekondari ya wasichana Loleza.
Akiongea kabla ya kuanza kwa mnada huo mhakiki wa mali za Serikali Bw.Simon Njoka aliweka wazi vigezo na masharti ya minada ya serikali ikiwemo kulipa asilimia 25 pindi mteja anapofanikiwa kuusimamisha mnada kwa kufikia bei iliyoshindwa kufikiwa na wengine na kumalizia malipo ndani ya siku kumi na nne kisha kuchukua mali ndani ya siku saba baada ya kumalizia malipo.
Kwenye mnada huo ulioendeshwa na Mhakiki Mkuu wa mali za Serikali Halmashauri ya Jiji la Mbeya imeuza vifaa mbalimbali ikiwemo mtambo wa kutengenezea miundombinu ya barabara,magari,majiko ya umeme ,vyerehani na kompyuta ambavyo vyote katika mnada huo wa awamu ya kwanza vimepata wateja.
Baadhi ya wateja waliofanikiwa kununua mali katika mnada huo Bw.Kato Martin ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Mbeya na Mhakiki Mkuu wa mali za serikali kuendesha kwa ukweli na uwazi shughuli hiyo kwa kuzingatia masharti na miongozo na kupata wateja kwa haki bila upendeleo kama ambavyo imekuwa ikijitokeza katika baadhi ya minada mingine.
Naye Bw.Andogwisye Mwamelo mteja ambaye hakubahatika kununua mali kwa kushindwa kupanda dau kwenye mnada wa awamu ya kwanza amesema ameridhishwa na uendeshwaji wa mnada huo kwa vile umezingatia haki na uwazi kama inavyotakiwa na masharti waliyotangaziwa awali kabla ya kuanza kwa zoezi hilo.
Mhakiki Mkuu wa mali za Serikali Bw.Simon Njoka ameongeza kuwa mnada huo awamu ya pili unatarajia kuendelea kesho kwenye eneo la Dampo Nsalaga ambapo yatauzwa magari na mali nyingine kwa kuzingatia sheria ,kanuni na taratibu za uendeshwaji wa minada ya serikali na amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika mnada huo wa hadhara.
Mbalizi Road near TTCL Offices
Anuani ya Posta: 149 Mbeya
Simu: +25525252502372
Simu ya Kiganjani: +255 25 2502563
Barua Pepe: cd@mbeyacc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya City Council . All rights reserved.