MKOA WA MBEYA WAJIPANGA KUZUIA NA KUPAMBANA NA MADAWA YA KULEVYA
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mh Amos G Makalla amekutana na Kamati zote za Ulinzi na usalama kutoka katika Wilaya zote za Mbeya,Wakuu wa vitengo mpakani Kasumulu, Wakuu wa vitengo TAZARA, Wakuu wa Uwanja wa Ndege Songwe, Wakuu wa Vituo vya Polisi,Waganga wakuu,Maafisa Elimu na Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Mbeya. Katika kikao kazi hicho Mh Makalla alitoa maelekezo muhimu ya namna ya kupambana na kutokomeza madawa ya kulevya katika Mkoa wa Mbeya na katika maeneo ya mipakani.
Mh Makalla aliwataka viongozi hao kumuunga mkono Waziri Mkuu Mh Kassim Majaliwa katika upambanaji wa madawa ya kulevya kwakuwa yeye ni mwenyekiti aliyepewa dhamana ya kusimamia suala hili na kuhakikisha Taifa linakuwa na kizazi salama kisichokuwa na waathirika ama watumiaji wa madawa ya kulevya.
Mh Makalla alisisitiza mambo makuu nane ambayo amewataka wahusika kuhakikisha wanasimamia kwa weledi kama jinsi ambavyo ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyosimamia na kutaka wananchi kupinga kwa bidii zote matumizi ya madawa ya kulevya.
1. Kamati ya Ulinzi na Usalama na vyombo vyote vihakikishe vinabeba dhamira ya dhati ya kuchukia madawa ya kulevya.
2. Awaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola katika mapambano ya madawa ya kulevya.
3. Aagiza agenda ya madawa ya kulevya iwe ya kudumu katika kila muhtasari utakao andikwa katika kila kikao.
4. Aagiza vyombo vyote vya ulinzi na usalama hususani vilivyopo mipakani kuhakikisha wanalinda na kuimarisha usalama katika maeneo yao ya kazi.
5. Vyombo vya Ulinzi na Usalama vinajua namna ya kukamata na kuchunguza hivyo wafanye kazi kwa weledi bila kumwonea mtu.
6. Madaktari wahakikishe wanatoa huduma pindi waathirika wa madawa ya kulevya watakapofika katika maeneo yao ya kazi na kuhitaji huduma ya kitabibu.
7. Maafisa Elimu wahakikishe wanatenga vipindi kwaajili ya kuwafundisha wanafunzi madhara ya matumizi ya madawa ya kulevya ili kuwaepusha kujiingiza katika matumizi hayo.
8. Aagiza wanahabari kuhakikisha jamii inaelimishwa juu ya madhara ya madawa hayo kwakuwa wao ndio walezi wa vijana ambao wengi wao wamekubwa na tatizo hili la matumizi ya madawa haya.
Nae Dr Paul Lawala toka Hospitali ya Mkoa alieleza mbele ya Mkuu wa Mkoa kuwa watumiaji wa madawa ya kulevya katika Mkoa wa Mbeya waliopokelewa katika hospitali hiyo kwaajili ya kupatiwa matibabu kwa mwaka 2016 ni jumla ya wagonjwa 483, “idadi hii imezidi kuongezeka kwa kila mwaka kwa miaka mitatu iliyopita kwa mfululizo nah ii ni ishara kuwa watumiaji wa madawa haya wanaongezeka kila siku kwa Mkoa wetu”alisisitiza
Nae RPC alisema mpaka sasa kuna jumla ya makosa 77 yanayohusisha madawa ya kulevya na kutaja maeneo vinara kwa matumizi ya madawa ya kulevya katika Jiji la Mbeya kuwa ni pamoja na Nonde, Ilomba, Soweto na Uyole na katika Wilaya ya Chunya alitaja makongorosi na kwa Rungwe ni Kiwira na Ushirika wakati Mbarari alitaja Ubaruku na Rujewa nakumalizia na Mji wa Mbalizi . Akihitimisha kikao kazi hicho Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Ndugu Zakaria Nachoa aliwaasa watendaji wa Kata kuhakikisha wanasimamia upigaji vita wa madawa haya katika maeneo yao ya kazi na kuhakikisha wanakomesha matumizi yake.
Mbalizi Road near TTCL Offices
Anuani ya Posta: 149 Mbeya
Simu: +25525252502372
Simu ya Kiganjani: +255 25 2502563
Barua Pepe: cd@mbeyacc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya City Council . All rights reserved.