TAARIFA YA UJENZI WA MRADI WA MAJI WA IZIWA
Mradi huu ni miongoni mwa miradi sita ya maji iliyotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya yenye jumla ya gharama ya Shilingi za Kitanzania 2,197,138,713.64 katika kipindi cha mwaka 2007 hadi 2018 katika kata za pembezoni mwa Jiji ambazo ni Ilomba (Ituha na Tonya), Iziwa, Itagano, Mwansekwa, Nsoho na Tembela.
Ujenzi wa mradi huu unatekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya na ulianza na usimamizi chini ya Mtaalamu Mshauri COWI TANZANIA LTD kwa sehemu na Halmashauri imesimamia hadi kukamilika kwake. Ujenzi wa mradi huu ulianza kutekelezwa na Mkandarasi EXTREME ENGINEERING COMPANY LTD na kukamilishwa na Mkandarasi J.O ENTERPRISES LTD baada ya Mkandarasi wa awali kushindwa kuendelea na kazi.
Ujenzi wa mradi huu ulianza mnamo tarehe Agosti, 2013 na ulitarajiwa kukamilika ndani ya mwaka mmoja lakini ilishindikana kukamilika kwa wakati kutokana na changamoto mbali mbali zikiwemo ukosefu wa fedha na kufariki kwa Mkandarasi wa awali.
Mpaka kukamilika kwa mradi huu ujenzi utagharimu jumla ya Shilingi za Kitanzania 373,430,630/= ambazo ni fedha kutoka Serikali Kuu. Hadi sasa mradi umetumia kiasi cha Shilingi za Kitanzania 364,094,864.25 na kiasi kilichobaki cha Shilingi za Kitanzania 9,335,765.75 ni fedha zilizobaki kama fedha za zuio.
Wananchi wameweza kuchangia jumla ya Shilingi za Kitanzania 3, 200,000/= katika mfuko wa mradi huu fedha ambazo zitatumika katika uendeshaji na matengenezo ya mradi.
Kazi zilizofanyika mpaka sasa ni ujenzi wa banio la maji, Ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji lenye ukubwa wa mita za ujazo 225 (sawa na lita 225,000) na kuzungushia wigo wa waya, Ujenzi wa matenki 2 ya kupunguza msukumo wa maji yenye ujazo wa mita za ujazo 4 kila moja, Ulazaji wa mabomba kwa jumla ya Kilometa 10.56 na ujenzi wa vituo 24 vya kuchotea maji. Mradi huu umekamilika na huduma ya maji inapatikana. Mradi upo katika muda wa matazamio wa mwaka mmoja kuanzia tarehe 01/03/2018.
MADHUMUNI YA MRADI
Madhumuni ya mradi huu ni kuboresha huduma ya maji na kuongeza idadi ya watu wanaopata huduma ya maji safi kwa wanachi waishio pembezoni mwa Jiji la Mbeya.
MANUFAA YA MRADI
Manufaa ya mradi huu wa maji ni kupunguza vihatarishi vya matumizi ya maji yasiyo safi kama vile magonjwa ya mlipuko n.k. kwa wananchi watakaonufaika na mradi huu. Aidha mradi utachangia matumizi bora ya maji ambapo huduma ya maji itaweza kupatikana katika makazi ya watu.
WANUFAIKA WA MRADI
Mradi huu unatarajiwa kunufaisha wanawake na jamii kwa ujumla kwa kuwapunguzia muda wa kutafuta huduma ya maji mbali na makazi yao na kutumia muda wao katika shughuli za uzalishaji mali, hivyo kukuza uchumi wa kaya na jamii kwa ujumla. Mradi huu unatarajiwa kuwanufaisha jumla ya wakazi 6,502 wa kata ya Iziwa na sehemu ya Kata ya Nsoho (Mtaa wa Idunda).
Mbalizi Road near TTCL Offices
Anuani ya Posta: 149 Mbeya
Simu: +25525252502372
Simu ya Kiganjani: +255 25 2502563
Barua Pepe: cd@mbeyacc.go.tz
Copyright ©2018 Mbeya City Council . All rights reserved.